Wazazi katika kaunti ya Nakuru wametakiwa kuhakikisha watoto wao walio chini ya umri wa miaka mitano wanapata chanjo dhidi ya Polio katika kampeni iliyongoa nanga Jumamosi.
Waziri wa afya katika kaunti ya Nakuru Dkt Mungai Kabii katika mahojiano ya kipekee na mwanahabari huyu Jumatatu alisema kuwa chanjo hiyo ni muhimu katika kuzuia visa vya ulemavu.
Kwa mujibu wake, zoezi hilo linatarajiwa kukamilika Jumatano, na kwamba wazazi wanafaa kulikumbatia.
"Zoezi hili ni la umuhimu sana katika kupunguza visa vya ulemavu na ningependa kuwarai wakaazi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hii," alisema Kabii.
Matamshi sawia yalitolewa na mwakilishi wa walemavu katika bunge la kaunti ya Nakuru Bi Emmah Mbugua.
Katika mahojiano kwa njia ya simu kuhusiana na zoezi la chanjo dhidi ya Polio, alisema kuwa ni zoezi la maana na wazazi wanafaa kulichukulia kwa uzito.
"Mimi kama mwakilishi wa walemavu, langu ni kuwahimiza tu wazazi wahakikishe watoto wao wanapata chanjo hii," alisema Mbugua.