Waziri wa ardhi na makazi katika serikali ya kaunti ya Nyamira Richard Mareri amewaonya vikali wamiliki wa nyumba dhidi ya kujenga nyumba za kibiashara karibu na barabara.
Akihutubia wakazi wa Ikonge siku ya Jumatatu, Mareri alisema kuwa serikali ya kaunti ya Nyamira itawachukulia hatua za kisheria wamiliki watakaopatikana kujenga nyumba za kibiashiara karibu na barabara za serikali.
"Kuna watu hasa wamiliki wa nyumba za kiabiashara walio na mazoea ya kujenga nyumba zao karibu na barabara za serikali, hali ambayo ni kinyume na sheria za nchi, na wacha wajue kwamba serikali itawachukulia hatua kali za kisheria," alisema Mareri.
Mareri aliongezea kusema kuwa huenda serikali ikalazimika kufutilia mbali leseni za mhandisi yeyote wa miundomisingi atakayepatikana kuhusika na uidhinishaji wa miradi hiyo.
"Inashangaza sana kwamba kuna wahandisi wanaohusika na kuidhinisha miradi ya ujenzi wa nyumba za kibiashara zinazojengwa barabarani na kwa kweli huenda serikali ikalazimika kufutilia mbali leseni zakuhudumu za wahandisi wahusika," aliongezea Mareri.
Picha: Waziri wa ardhi na makazi katika serikali ya kaunti ya Nyamira Richard Mareri. Amewaonya vikali wamiliki wa nyumba dhidi ya kujenga nyumba za kibiashara karibu na barabara. WMaina/Hivisasa.com