Waziri wa mashamba na makazi kwenye serikali ya kaunti ya Nyamira Richard Mareri amewaonya vikali wawekezaji wa kibinafsi dhidi ya kunyakua ardhi za umma katika kaunti hiyo.
Akiwahutubia wanahabari wakati wa kutembelea miradi mbalimbali ya soko zinazojengwa na serikali ya kaunti ya Nyamira siku ya Jumatatu, Mareri alisema kamwe wanyakuzi wa kibinafsi hawataruhusiwa kunyakua ardhi za umma.
"Ni onyo kwa wawekezaji wa kibinafsi walio na mazoea ya kunyakua ardhi za umma kinyume na sheria, na wacha wajue kwamba kamwe serikali haitoketi na kuwatazama," alisema Mareri.
Mareri aidha aliongeza kwamba serikali ya kaunti hiyo itatumia millioni 70 ili kumalisha ujenzi wa soko tano zitakazosaidia wafanyabiashara kuendesha shughuli zao bila matatizo kote Nyamira.
"Tuna mipango ya kumaliza ujenzi wa soko tano zikiwemo Magwagwa, Mokomoni Ikonge, Nyamusi na zingine kwa matumizi ya shillingi millioni 70 ili kuwawezesha wafanyabiashara kuendelesha biashara zao bila matatizo," aliongezea Mareri.
Picha: Waziri wa mashamba na makazi kwenye serikali ya kaunti ya Nyamira Richard Mareri. Amewaonya vikali wanyakuzi wa ardhi katika kaunti hiyo ya Nyamira. WMaina/Hivisasa.com