Waziri wa barabara katika kaunti ya Nyamira Janet Komenda amekanusha vikali madai ya mwakilishi wadi wa Bogichora Beutah Omanga kuwa wizara yake imepuuza eneo lake kwa kutokarabati barabara nyingi ambazo ziko katika hali mbovu.
Haya yanajiri baada ya Omang'a kulalamikia hali mbaya ya barabara katika eneo lake, huku akiikosoa wizara ya barabara kwa kutojali eneo lake.
Akihutubu kwenye shule ya upili ya wasichana ya Sironga siku ya Alhamisi, Komenda alisema kuwa wizara yake imekuwa ikikarabati barabara mbalimbali katika kaunti hiyo.
"Hii dhana aliyonayo mwakilishi wa wadi ya Bogichora kwamba wizara ya barabara na miundomisingi haijakuwa ikishughulikia ukarabati wa barabara katika eneo wadi yake sio la kweli kwa kuwa tumekuwa tukizikarabati barabara, ila kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha ndio sababu iliyotufanya kusitisha ukarabati huo kwa muda," alisema Komenda.
Komenda aidha aliongeza kusema kuwa wizara yake imefanikiwa kuezeka taa katika soko la Ikonge, Kebirigo na Keroka, huku akiwasihi wakazi wa maeneo hayo kutojihusisha na uharibifu wa taa hizo.
"Tayari tumeezeka taa za sola kwenye soko la Ikonge, Kebirigo na Keroka ili kuwawezesha wafanyabiashara kuendesha shughuli zao hadi usiku, ila ningependa kuwarahi wananchi kutojihuzisha na uharibifu wa taa hizo," aliongezea Komenda.