Waziri wa barabara na miundomisingi katika serikali ya  kaunti ya Nyamira Janet Komenda amewaomba wanakandarasi wanaokarabati barabara katika kaunti hiyo kumaliza ukarabati wa barabara kwa wakati. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano kwa njia ya simu mapema Jumatano, Komenda alisema kwamba yafaa wanakandarasi wanaokarabati barabara katika kaunti hiyo wamalize ukarabati kwa mapema ili kuruhusu shughuli za uchukuzi kuendelea bila matatizo. 

"Watu wengi hasa wakulima na wafanyabiashara hupata wakati mgumu sana wanaposafirisha mazao na bidhaa zao kutokana hali mbaya ya barabara, na ndio maana nawahimiza wanakandarasi kuweka mikakati ya kuhakikisha wamemaliza ukarabati wa barabara kwa wakati," alisema Komenda. 

Komenda aidha aliwasihi wakazi wa maeneo mbalimbali katika kaunti hiyo, ambapo barabara zinapanuliwa kutopinga hatua hiyo kwani inahujumu maendeleo.

"Kuna ripoti zinazonifikia kwamba baadhi ya wakazi wa maeneo ambapo barabara zinakarabatiwa wanapinga upanuzi huo na ndio maana ningependa kuwarahi kuepukana na tabia hiyo kwa kuwa inahujumu maendeleo," aliongezea Komenda.