Samaki baada ya kuvuliwa. /Nicholas Ngumbao

Share news tips with us here at Hivisasa

Waziri wa viwanda Aden Mohammed amesema kuwa idadi kubwa ya samaki wa kuagizwa  wamekuwa wakiingia humu nchini kutoka taifa la Uchina kwa sababu Kenya haizalishi samaki wengi ikilinganishwa na jinsi wakenya wanahitaji samaki.

Akizungumza mjini Mombasa katika kongamano la bunge kuhusu  biashara, viwanda na mashirika katika hoteli moja, waziri Mohammed alisema kuwa kukosekana kwa chakula cha samaki kumechangia pakubwa hali hiyo.

Kwa upande wao, wafanyibiashara wa kuuza samaki wamekuwa wakilalamika kuwa samaki wanaotoka nje wamekuwa wakitozwa ada ndogo na hivyo kuharibu biashara ya samaki nchini.

Mjini Mombasa, wafanyibiashara wa samaki wanasema kuwa samaki aina ya tilapia kutoka uchina anauzwa kwa bei nafuu sana na hivyo wao kukosa soko la samaki wao.

‘‘Wafanibiashara waliokuwa wakinunua samaki kutoka kwetu hawako sasa. Eneo la Majengo ndilo lilikuwa soko kubwa la samaki lakini siku hizi hatupati  wateja,’’ Alisema Nobert Otieno, mmoja wa wafanyibiashara wa kuuza samaki.

Kwa mfano samaki aina ya Tilapia mwenye uzani wa kilo moja  kutoka uchina anauzwa kati ya shilingi 150-300 huku wa Kenya akiuzwa kwa bei ya shilingi 400.