Katibu mkuu wa chama cha ODM Ababu Namwamba amewaomba wanasiasa kuweka siasa kando na kuunga mkono viongozi walio mamlakani kuleta maendeleo katika wananchi wa Kenya.
Namwamba alisema kuna baadhi ya wanasiasa humu nchini wanaendelea kufanya siasa badala ya kuweka masuala hayo kando na kuwapa fursa viongozi ili kutekeleza maendeleo kwa wananchi.
Akiongea siku ya ijumaa katika eneo la Itare eneo bunge la Bomachoge, Kaunti ya Kisii, wakati alikuwa anaendesha mradi wa 'Tokelezea ID' wa kuwahimiza vijana na wananchi wote kupata vitambulisho ambavyo vitawawezesha kuchagua viongozi wa maono siku za usoni, Namwamba alisema kwa sasa maendeleo ni muhimu kuliko siasa.
“Nawaomba wanasiasa wote muweke siasa kando ili viongozi wafanye maendeleo katika sehemu zote za nchi. Kama unahitaji kuwania kiti chochote kiwe cha uakilishi wa wadi, ubunge, seneta, gavana na hata kile cha urais, subiri hadi mwaka wa 2017 lakini kwa sasa tufanye maendeleo kwanza,” alisema Namwamba.
Namwamba alisema tangu serikali za ugatuzi zianzishwa nchini, mabadiliko yamekuwa katika sehemu za mashinani na kukiri kuwa wataendelea kuunga mkono serikali za ugatuzi na kuzitetea kuongezewa pesa ili maendeleo kuinuka zaidi hasa sehemu za mashinani.
Aidha, aliomba serikali kuheshimu mahakama kuu nchini na kuwalipa walimu nyongeza yao ya mishahara.