Shughuli ya kupimwa ugonjwa wa saratani bila malipo hii leo (Jumatatu) umeanza katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kisii huku watu wengi wakijitokeza katika shughuli hiyo.
Baadhi ya watu hao wamewaomba wasimamizi wa sekta ya afya katika hospitali hiyo kuongeza siku tatu zaidi ya shughuli hiyo ili kila mmoja wao apate nafasi ya kupimwa.
Kutokana na idadi kubwa ya watu waliojitokeza huku wengine wakilala hospitalini wakisubiri shughuli hiyo shughuli kuanza, ilibidi kila mtu kupewa nambari ya kujua orodha yake kwa kuwa walikuwa zaidi ya watu 1,000 na wengine huku wengine wakizidi kufika hapo.
“Ningependa kuwaomba wasimamizi wa sekta hii ya afya kuongeza siku kama tatu ili kila mmoja wetu afikiwe na kupimwa kwa kuwa tuko wengi na kila mmoja anahitaji kupimwa,” alihoji mzee Johnstone Kerogo.
Kupimwa kwa ugonjwa huo wa saratani uliandaliwa na Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kisii wakishirikiana na madaktari wa Hospitali ya BLK kutoka India.
Wengine waliofika pele kupimwa walitoka Kaunti jirani kama Nyamira, Migori, Siaya miongoni mwa nyinginezo.
“Niliamka mapema kutoka kwangu Mosobeti ilioko Kaunti ya Nyamira ili kufika hapa mapema nami nipimwe ndio nibaini kama nina ugonjwa wa saratani na kama sina bado najua kuna mafunzo tutapewa na yatanisaidia,” alihoji Milka Bosire.
Kwa mujibu wa mkuu wa idara ya Afya katika Kaunti ya Kisii Sarah Omache, walifikiana na madktari kutoka India ili kuwasaidia watu kwa kuwapima na kubaini kama wana ugonjwa wa saratani kwani saratani ni janga kubwa duniani na ni ugonjwa unaostahili kugunduliwa mapema kabla viwango vyake kuwa vikubwa kwenye damu ya binadamu.