Wamiliki wa majumba ya kibiashara mjini Nakuru wamepewa muda wa miezi mitatu kuhakikisha kuwa majumba yao yanapakwa rangi upya.
Waziri wa ardhi, nyumba na mipango katika kaunti Rachael Maina alisema kuwa hiyo ni mojawapo wa mikakati ya serikali ya kuunadhifisha mji wa Nakuru.
Akihutubia wanahabari ijumaa asubuhi afisini mwake, Maina alisema kuwa wamiliki wa majumba ambao hawatatii agizo hilo baada ya miezi mitatu watachukuliwa hatua za kisheria kulingana na sheria za kaunti.
“Tunatoa amri kwa wenye majumba kuhakikisha kuwa majumba yao yanapakwa rangi upya kwa muda wa miezi mitatu, na wale ambao hawatakuwa wamefanya hilo, basi watakabiliwa kulingana na sheria zetu za mji,” alisema Maina.
Maina aliongeza kuwa kuna majumba katika mji yaliyojengwa siku za ukoloni ambayo alisema yanafaa kubomolewa na kujengwa kulingana na mipango mipya ya mji.
“Tumeunda sheria mpya zitakazoongoza sekta ya ujenzi katika mji yote katika kaunti ya Nakuru na katika sheria hiyo tunapendekeza kwamba majumba yote ambayo yalijengwa nyakati za ukoloni yabomolewe na kujengwa upya ili yaambatane na mipango yetu,” alisema.
Serikali ya kaunti ya Nakuru imezindua mikakati ya kuusafisha mji wa Nakuru ili kuurejesha katika kiwango cha kuwa mji msafi zaidi katika eneo la Afrika mashariki.