Wakaazi wa eneo la Songhor kaunti ndogo ya Muhoroni wamehimizwa kuwafunga mbwa wao nyakati za mchana.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi hao pia wameonywa kuwa mbwa watakaoonekana wakirandaranda kwenye soko na barabarani wenyewe watachukuliwa hatua.

Agizo hilo lilitolewa siku ya Alhamisi na mkuu wa afya katika eneo hilo, Suzan Adimo ambaye alisema kuwa mbwa wanaorandaranda barabarani na soko za Songhor na Achego wanahatararisha maisha ya wakaazi mbali na kusababisha hali mbaya ya mazingira kwa kusambaza kinyesi kwenye maeno ya soko.

“Tafadhalini nawasihi wenyeji wa hapa muwafungie mbwa wenu nyakati za mchana ili kupunguza visa vya watu kushambuliwa na mbwa wakiwa kwenye shughuli zao mchana,” alisema Adimo.

Mkuu wa mtaa wa Oneno Wang’ Albert Obonyo alisema kwamba ni mara nyingi akiwaonya wakaazi walio na mbwa wakali kufuata sheria na maagizo yanayohusiana na ufugaji wa wanyama aina hao.

Alisema kuwa wengi walipuuza agizo hilo na sasa madhara yanaendelea kuongezeka wakati watu wanaposhambuliwa kila mara na wanyama hao.

Wengi kwenye kikao hicho walitoa lalama zao kuhusu kuachilia mbwa wakali kurandaranda vijijini na kwenye soko ambapo wanao wadogo wameathirika kwa kushambuliwa na wanyama hao wakali, wengine wakiwa wanaenda shule nyakati za asubuhi.