Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wenye nyumba katika kaunti ya Nakuru, hususan katika mitaa ya Mabanda, watachukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa kudaiwa kuchangia maradhi yanayotokana na uchafu.

Afisaa wa afya wa kaunti ya Nakuru Samuel King’ori ametishia kuwachukulia baadhi ya wenye nyumba hatua kwa kukosa kuwatengezea wapangaji vyoo na kupelekea wapangaji kutumia makaratasi ya plastiki kama choo 'Flying Toilets' inayosababisha vinyesi kutapakaa katika maeneo hayo.

Kutokana na jambo hilo, King'ori amesema kuwa kuna hatari ya kuzuka upya kwa maradhi ya kipindupindu, ikizingatiwa kuwa, huu ni msimu wa mvua ya Elnino.

Aidha, King'ori amesisitiza kuwa ametoa makataa ya siku ishirini na moja kwa wenye nyumba hizo wawe wametengenezea wapangaji wao vyoo la si hivyo, ploti hizo zikafungwa na wenye nyumba hizo kufunguliwa mashtaka.

King’ori ambaye ameonekana kugadhabishwa na hali hiyo, ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa makataa hayo, wataanza kuzuru kila mtaa wa kaunti hiyo li kutathmini hali.

Hata hivyo, King’ori ametoa wito kwa wapangaji kuwasiliana au hata kupiga ripoti katika ofisi yake ili wenye nyumba ambao wanakiuka amri hiyo wakabiliwe kisheria.