Wamiliki wa vibanda vya maji katika Kaunti ya Mombasa, chini ya mwavuli wa ‘Mombasa Water Kiosk Operators Association’ wameitaka serikali ya kaunti kusitisha oparesheni ya kufunga vibanda vyao kwa madai kuwa wanawauzia wakaazi maji kwa bei ghali.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao Ben Ndege, wafanyibiashara hao waliaanda mkutano wa amani mjini Mombasa siku ya Alhamisi, ambapo walimtaka Gavana wa Mombasa Hassan Joho kuwaagiza maafisa wa maji mjini humo kukoma kuwahangaisha, huku wakishikilia kuwa hawajaongeza bei ya maji.
“Tunauza maji shilingi tano kwa kila mtungi kulingana na ada tunazotozwa na kampuni ya maji ya Mombasa. Leo hii tunalaumiwa kuwa tumeongeza bei ya maji,” alisema Ndege.
Wafanyibaishara hao aidha walisema kuwa wenye mikokoteni mjini humo ndiyo wanaofaa kulaumiwa kwa kuwa wananua maji shilingi tano kisha wanawauzia wakaazi kwa shilingi 20 kwa kila mtungi, japo kwa maelewano.
Haya yanajiri wiki chache tu baada ya Joho kusema kuwa serikali ya kaunti itafunga vibanda vyote vya kuuza maji mjini Mombasa ambavyo vinadaiwa kuuza maji kati ya shilingi 20-30 kwa mtungi mmoja, badala ya shilingi tano.
Tayari oparesheni ya kufunga vibanda hivyo imeanza ambapo maeneo ya Changamwe, Jomvu na Mikindani yameripotiwa kuathirika zaidi.