Wamiliki wa vichinjio vya kibinafsi mjini Naivasha wameonywa dhidi ya kuwachinja ng'ombe walioathirika na ugonjwa wa kuoza kwa miguu na midomo katika eneo hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa mkuu wa mifugo katika eneo hilo, Enos Amuyunzu, ameonya kuwa yeyote atakaye patikana akichinja mifugo haswa ng’ombe alioathirika atakamatwa na kushtakiwa.

Akiongea jumatatu asubuhi wakati wa shuguli ya kuwachanja mifugo mjini Naivasha,Amuyunzu alisema kuwa ni sharti kila mfugo anayewasilishwa katika vichinjio akaguliwe na daktari wa mifugo wa serikali kabla ya kuchinjwa.

“Kuna mifugo wengi ambao wameathirika na ugojwa wa miguu na midomo na kuna baadhi ya wenye vichinjio ambao bila kujali wanawachinja mifugo kama hao na kuuza nyama hiyo kwa wenye mabucha na tunataka kuwaonya kuwa tukiwapata basi sheria itafanya kazi yake. Ni sharti kila mfugo anayepelekwa kwenye kichinjio akaguliwe na daktari wa serikali na adhibitishwe kuwa salama kabla ya kuchinjwa,” alisema Amuyunzu.

Amuyunzu vileviel aliwataka wafugaji wote kuwasilisha mifugo wao katika vituo vya kuepeana chanjo ili wapate chanjo dhidi ya ugonjwa huo ambao husambaa kwa kasi sana.

Aliwarai wafugaji kuchoma mizoga ya ngombe wanaofariki kutokana na ugonjwa huo ili kukinga mifugo wanaobaki.

“Iwapo kuna mfugo yeyote ambaye amefariki kutokana na ugonjwa huu ni vyema huo mzoga uchomwe na mkome kula nyama hiyo kwa sababu ni hatari kwa afya ya binadamu,” alisema.

Ugonjwa wa miguu na midomo ulizuka Mjini Naivasha mwaka jana hali iliyopelekea serikali kuweka marufuku ya kusafirisha mifugo kutoka na kuingia wilayani humo na pia kuanzisha shuguli ya kuwachanja mifugo katika Kaunti nzima ya Nakuru.