Wakazi na wafanyabiashara katika eneo la Likoni wanawashtumu madereva wa malori pamoja na wahudumu wenza kwa kueneza ukahaba na kujihusisha na vitendo vya kimapenzi kiholela katika mtaa huo hasa nyakati za usiku.
Wakazi hao pamoja na baadhi ya wafanyabiashara, wamedai kuwa malori hayo ambayo yamekuwa yakiegeshwa kando kando ya barabara ya kutoka Ukunda kuja katika barabara ya kuelekea kivuko cha Likoni, yamezua mjadala ambapo wamewanyoshea madereva na wahudumu kidole cha lawama kwa kuwatumia wasichana kimapenzi inapowadia jioni kuanzia saa moja usiku.
Kulingana na mama Amina Athmani ambaye ni muuzaji wa samaki katika eneo hilo la soko la Likoni aliweka bayana kuwa madereva hao kwa mara kadhaa wameonekana wakiwa na wanawake wa kuuza miili mtaa huo na kutumia magari yao kama madanguro na hata kwa kile alichotaja kuwa ukosefu mkubwa wa adabu baadhi yao wamekuwa wakiingia chini ya malori hayo na kutosheleza ashiki zao.
“Si peke yangu nimelalama ila kila mmoja ambaye hufanya shughuli za kibiashara hapa Likoni amejionea angaa mara moja vitendo vya madereva hao na wahudumu wenzao na vitendo hivi vimekithiri sana kila mara magari haya yanapoegeshwa hapa kando ya barabara,” alilalama mfanyabiashara huyo.
Matamshi hayo yaliungwa mkono na wengi wa wafanyibiashara wengine ambao waliongea na mwandishi huyu siku ya Jumatano na kusema kuwa vitendo hivyo havijawafurahisha wakazi wa eneo hilo na kuitaka serikali ya Kaunti kuchukua hatua dhidi ya wahusika hao.
Hata hivyo mmoja wa madereva hao ambaye aliongea na makala haya, Suleiman Jumaine ambaye ni raia wa Tanzania alitetea madereva wenzake akisema kuwa wengi wao hutoka nchi jirani na kitambo wakifika eneo la Kivuko huwa wamechoka na huegesha malori hayo kupumzika wakingojea kuelekea bandarini kuchukua shehena zao japokuwa alikubali kuwa watu wote hawako sawa na kuna wale madereva ambao watajihisisha kwenye vitendo hivyo.