Vijana na kina mama kutoka Wadi za Kibuyuni B na Dimbwini, eneo bunge la Likoni, wametishia kufanya maandamano siku ya Alhamisi kulalamikia kutohusishwa kwenye mradi wa kukarabati barabara za sehemu hiyo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano wakiongozwa na Mohammed Juma, wakaazi hao walisema kuwa mwanakandarasi ambaye alipewa jukumu la kusimamia ujenzi wa barabara hizo ndogo za kuunganisha mitaa hiyo kuenda na kutoka eneo la feri ya Likoni, amewaajiri watu ambao wanaaminika kutoka kwenye jamii yake.

Juma alisema kuwa mwanakandarasi huyo hajamhusisha kijana wala mkaazi yeyote kutoka sehemu hiyo na kutaja hatua hiyo kuwa ya ubaguzi mkubwa.

Wakaazi hao walisema kuwa hawatakaa na kuangalia wakinyimwa haki zao za msingi za kupata hata kazi nyepesi kama hizo ambazo hazihitaji ujuzi wa kiufundi.

“Tuna haki ya kupewa kazi hapa. Kwani ni vipi mtu anaweza kutoa watu kutoka kaunti nyingine kuja kufanya kazi hapa ilhali sisi wakaazi wa eneo hili hatujapewa hata kazi za kubeba mchanga,” alisem mkaazi mmoja.

Wenyeji hao waliapa kufanya maandamano siku ya Alhamisi kulalamikia hatua hiyo na kumtaka mbunge wao Mwalim Mwahima kuangalia swala hilo na kulitafutia suluhu.

Hatua za mwandishi huyu kuongea na msimamizi huyo ziligonga mwamba kwani alikuwa ameondoka kulingana na ripoti kutoka kwa kijana mmoja aliyekuwa akihudumu kwenye mradi huo.