Wakaazi wa mji wa Molo wamelalamika vikali kuhusiana na hali mbaya ya chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya wilaya ya Molo.
Wakiongozwa na diwani wa zamani wa eneo hilo, Njenga Matendo, wakaazi hao walisema chumba hicho hakina vifaa vya kutosha vya kuendeleza shughuli za kuhifadhi wafu.
“Hiki chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya wilaya ya Molo kiko katika hali mbaya. Kina uwezo wa kuhifadhiwa mili tisa tu licha ya kuwa kinatumika na wakaazi wa kaunti nne ndogo; Molo, Kuresoi Kusini, Kuresoi kaskazini, Londiani na Njoro,” akasema Matendo.
Kwa sasa wakaazi wanaitaka serikali ya kaunti ya Nakuru kuhakikisha chumba hicho kimeafikia viwango vinavyokubalika vya afya.
Matendo pia alisema kuwa mazingira ya chumba hicho ni ya kutisha jambo ambalo linachangiwa sana na uvundo unaotoka humo ndani.
“Mahali hapa ni pa chafu sana. Jambo hili lina changiwa sana na shida ya maji ambayo imekumba kaunti yetu,” asema Matendo.
Matendo amesema chumba hicho hakifai kuwa kinatumika iwapo kanuni za afya hazitafuatiliwa kikamilifu akisema wadudu kama vile siafu na panya hutatiza shughulii katika ufuo wa hospitali hiyo.
Kwa sasa wakaazi hao wanaiomba serikali ya ngatuzi la Nakuru kujenga chumba kingine ambacho kitakuwa na vifaa vya kisasa.
Wakaazi hao pia wameteta kuwa shamba la kuwazika wafu ambalo lilikuwa limetengwa na serikali katika eneo hilo limenyakuliwa na mwekezaji wa kibinafsi.
kwa sasa wanataka serikali ifanye juhudi na ilinyakue shamba hilo.