Seneta wa Kaunti ya Bungoma amemtaka kinara mwenza wa mrengo wa Cord Raila Odinga kusitisha azma yake ya kuwania urais mwaka wa 2017 na kumuunga mkono.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza siku ya Jumamosi katika hafla ya mazishi huko Kakamega, Moses Wetangula alimtaka Raila kumuunga mkono kwa kumpa nafasi ya kupeperusha bendera ya Cord.

"Wakati umefika kwa Bwana Raila kurudisha shukrani kwa jamii ya Waluhya. Mgombea wa urais wa muungano wa Cord mwaka wa 2017 anapaswa kutoka katika jamii ya Waluhya,” alisema Wetangula.

Aliongeza, "Kutoka enzi za babake Jaramogi Odinga, Waluhya wamesimama naye. Hivyo basi, itakuwa jambo la busara kwa Raila Odinga kuniunga mkono wakati huu kama njia ya kurudisha shukrani.”

Seneta huyo alisema kuwa jamii ya Waluhyia ndiyo ya pili nchini kote kwa idadi ya wapiga kura, na kuwa vinara wenzake wakimuunga mkono basi itakiwa rahisi kutwaa uongozi wa nchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa zamani wa Lugari Bwana Cyrus Jirongo, alipendekeza jamii ya Waluhya kuuhama mrengo wa Cord na kuunda chama chao cha kisiasa, kitakachowapa nguvu za kujitetea kisiasa.

Hata hivyo, Wetangula alipuuziia mbali ombi hilo na kusema kamwe hatakihama chama cha Cord.

"Nitakuwa wa kwanza kuunga mkono yeyote yule atakayeibuka mwenye sifa dhabiti za kupeperusha bendera ya Cord," alisema Wetangula.