Seneta wa Bungoma Moses Wetangula, alizindua azma yake ya kuwania urais hivi majuzi katika bustani la Muliro, kaunti ya Kakamega.
Wetangula, kama mwanasiasa yeyote , ana haki ya kufanya hivyo kikatiba kama njia moja ya kuwafahamisha wafuasi wake kuhusu azma yake.
Hisia nyingi ziliibuka kuhusiana na swala hilo, na kulifanya liwe kawaida, kulikuwa na hisia mseto.
Ingawa Wetangula ana nia ya kumrithi Uhuru Kenyatta kama rais wa jamhuri ya Kenya, hajahitimu kikamilifu kuipeperusha bendera ya muungano wa Cord, ingawa yeye pia ni kinara wa muungano huo.
Cord imekuwa ikiwapoteza wabunge hivi majuzi na hivyo kuna haja ya kuchagua mgombeaji thabiti atakayeihakikishia ushindi.
Ingawa Wetangula ana umaarufu katika uliokuwa mkoa wa magharibi, anakabiliwa vikali na upinzani kutoka kwa wanasiasa wa eneo hilo. Mfano ni gavana wake Kenneth Lusaka.
Na iwapo Musalia Mudavadi wa chama cha Amani National Congress atawania urais, basi itabidi Wetangula agawane kura za mkoa huo naye.
Wetangula amebuni umaarufu wa kutajika chini ya mwavuli wa Cord na hivyo uhakika wake wa kuwa rais haujakomaa.
Cord sasa ina kati ya Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kuchagua ni yupi atakayeipeperusha bendera yake, ikiwa ina haja ya kutwaa uongozi.