Wakaazi wa Omosocho-Gekomu katika eneo Bunge la Nyaribari Chache waliokaribu na barabara ya Kisii-Kilgoris wameghadhabishwa na tabia ya baadhi ya watu ambao wanaiba vizuizi vya mabati ambavyo vimeweka kando ya barabara ili kuzuia magari yanapoanguka katika eneo hilo.
Wakiongea siku ya Jumatatu katika mtaa wa Mwembe, baadhi ya wakaazi hao wamesema kuwa kuna wezi wa mabati hayo huku wakiwaonya kuwa siku yao zinahesabiwa na watakapokamatwa watachukuliwa hatua kali ya sheria.
Aidha, wamewaonya kuwa wanaotekeleza kitendo hicho wakome kwa kuwa mabati hayo yamewekwa hapo kwa ajili ya usalama wa barabara hiyo na kuongeza kuwa kando ya mabati hayo ni bonde kubwa kwa hivyo mabati hayo yanazuia uwezekano wa kupata ajali pakubwa.
“Mabati haya yaliwekwa na waliokarabati barabara hili kwa usalama wa barabara na sisi wenye tumejenga karibu na barabara hili kwa hiyo mabati hayo yanatusaidi hasa kuzuia magari yanapoanguka katika mahali hapa,” alisema Jonstone Nyakoiba mkaazi.
Kulingana na wao kuibiwa kwa mabati hayo ni kuweka maisha yao katika hali ya hatari kwa kuwa gari likipata ajali na kuanguka kwa bahati mbaya linawezafikia nyumba zao na kusababisha vifo.
“Mwaka jana Tulishuhudia gari moja ambalo lilianguka katika mahali hapa na kama si mabati haya yaliyolizuia kwa ukweli gari hilo lingefikia nyumba ya jirani yangu kwa hivyo ninaomba sekta ya barabara kuwatafuta watu hao na wakipatikana wachukuliwe hatua ya kisheria,” alisema Nyakoiba.
Duru za kuaminika ni kuwa wanaoshukiwa ni wale watu wanaofanya biashara za kununua chuma ndio wamechangia mabati hayo kuporwa.
Kwingineko wakaazi hao wameiomba Serikali ya Kaunti kuweka matuta katika barabara hiyo kwa kuwa magari yanayotumia barabara hilo, kwa mfano aina ya Probox, yanaendeshwa kwa kasi sana na watoto huvuka barabara hilo wakienda shuleni.