Mipango ya kumuondoa spika wa bunge la Kaunti ya Mombasa inaendelea kushika kasi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wapinzani wa Spika Thadius Rajwayi, wamesema kuwa hawatapumzika mpaka spika huyo ang'atuke mamlakani.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati ya fedha katika kaunti hiyo Mohamed Hatimy siku ya Jumanne, wawakilishi wa wadi hao walisema kuwa watawasilisha stakabadhi muhimu walionazo ambazo zinadhihirisha kuwepo kwa ufujaji na matumizi mabaya ya fedha katika bunge hilo.

Hatimy alisema kuwa hatapumzika kamwe mpaka Rajwayi aondolewe mamlakani.

Vikao katika bunge hilo vilikosa kuendelea siku ya Jumanne kufuatia kukosekana kwa fimbo maalum ya spika baada ya fimbo hiyo kuvunjika wiki iliyopita vurugu zilipozuka bungeni humo.

Huku hayo yakijiri, wanaomuunga mkono spika huyo walimkemea Bwana Hatimy kwa kile walichokitaja kama vita visivyo na msingi wowote.

Wafuasi wa Rajwayi walisema kuwa mgogoro huo unashuhudiwa kwa vile spika huyo amekuwa kikwazo kwa mipango ya wapinzani wake ya utumizi mbaya wa mamlaka.