Seneta wa Mombasa Hassan Omar ameyataja kama uvumi usio na msingi wowote madai kuwa chama cha Wiper katika siku za hivi majuzi kimekuwa kikishauriana na Ikulu.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza kwenye kikao na wanahabari katika makao ya Bunge mjini Nairobi siku ya Alhamisi, Omar, ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Wiper alisema kuwa hicho ni chama chenye uwezo wa kujitegemea na kuwa hakiwezi kuukubali ushauri kutoka kwa Ikulu.

Aidha, Omar aliwakashifu wabunge watatu walionukuliwa kutishia kuuhama muungano huo siku ya Jumanne akiwemo Joe Mutambu (Mwingi ya Kati), Richard Makenga (Kaiti) na Kisoi Munyao (Mbooni), huku akisema kuwa wabunge hao tayari walikuwa wakishirikiana na muungano wa Jubilee, hivyo vitisho vyao havikuwa na athari yoyote kwa Cord.

Wabunge hao ambao ni wanachama wa Cord mapema wiki hii walinukuliwa kwenye vyombo vya habari wakiwasuta viongozi wa chama cha Wiper kwamba wamekuwa wakishirikiana na Ikulu katika siku za hivi majuzi, madai ambayo kulingana na seneta wa Mombasa Hassan Omar hayana ukweli ndani yake.