Kinara wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka katika hafla ya awali. [Picha/ nation.co.ke]
Naibu kinara wa chama cha Wiper Shakila Abdalla amepinga madai kuwa kinara wa chama hicho Kalonzo Musyoka huenda akajiunga na chama cha Jubilee pindi atakapowasili humu nchini kutoka Ujerumani.Shakila ametaja uvumi huo kama propaganda na kusisitiza kuwa Kalonzo bado ni kigogo katika mrengo wa NASA.Shakila, ambaye alikuwa mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Lamu, amewataka Wakenya kupuzilia mbali uvumi huo ambao ameutaja kuenezwa na wafuasi wa Jubilee.Mwanasiasa huyo ametaja propaganda hizo kama njama ya Jubilee kutaka kusambaratisha mrengo wa NASA.“Hii ni njama ya Jubilee kutaka kugawanya na kusambaratisha upinzani,” alisema Shakila.Kwenye mahojiano na mwanahabari huyu siku ya Jumanne, Shakila alisema kuwa kwa sasa Kalonzo yuko nchini Ujerumani kwa shughuli za kibinafsi.“Kwa sasa Kalonzo yuko nje ya nchi kwa shughuli za kibinafsi. Hata hivyo, bado atasalia kuwa kigogo wa mrengo wa NASA,” alisema Shakila.Aliongeza kuwa Kalonzo atarudi humu nchini hivi punde na kuendelea na shughuli za mrengo wa NASA.Haya yanajiri wiki chache baada ya aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha Wiper Hassan Omar kujiondoa kutoka chama hicho na kujiunga na Jubilee.