Wanafunzi wakike kutoka Shule ya Upili ya St. Catherine iliyoko katika eneo la Ahero katika Kaunti ya Kisumu wameomba Serikali kuangalia masilahi ya wanafunzi wasichana kwenye shule zote nchini kwa kuwapa vifaa vya kukabiliana na hali yao ya hedhi.
Wakizungumza na Mwandishi huyu wakati alipowatembelea shuleni mwao mnamo jana Alhamisi, wanafunzi hao walielezea matatizo wanayoyapitia wakati wa hedhi kwa sababu za kukosa sodo za kuwakinga wakati kama huo.
Walisema kuwa wakati wa hedhi unapowadia hua hawana lingine zaidi ila tu kusalia nyumbani, kwa kuona haya kutangamana na wenzao huku wakiwa kwenye hali ngumu isiyowaruhusu kukaa darasani.
“Tunapoanza hedhi tunalazimika kusalia nyumbani wakati wenzetu wanapoendelea na masomo kwa kuwa tunaona haya kujiunga na wenzetu tukiwa ‘wachafu’ bila kujisitiri na sodo maanake wengi wetu hawana uwezo wa kununua sodo,” alisema Nancy Odoyo mmoja wa wanafunzi hao.
Lilian Apiyo naye alisema kuwa, “Ni hasara kubwa sana kwetu kukosa kuhudhuria darasa kwa mara moja au mbili kwa mwezi, kwa kuwa ni vigumu kujaza pengo la silabasi zinazotupita tikuwa nje.”
Wanafunzi hao sasa wameiomba Serikali pamoja na Mashirika zisizo za Kiserikalio kuingilia kati swala hilo na kutoa msaada wa sodo kwa wanafunzi wasichana kwenye shule za humu nchini ili kuweza kuokoa kisomo chao ikizingatiwa kuwa masomo ya mtoto wa kike kwa wakati mwingine huwa magumu kutokana na hatari kubwa walizo nazo za kuacha shule.
Ilifichuka kwamba idadi ya wanafunzi wengi wanaoacha shule hutokana na hali ya ukosefu wa vifaa muhimu wanavyohitaji na wala hawavipati, hali ambayo hufungua mianya ya kuhadaiwa na wanaume ambao huwaahidi kuwasaidia baada ya kushiriki nao mapenzi ambayo matokeo yake ni mimba za mapema, kuacha shule na kupata magonjwa hatari kama vile Ukimwi na yale ya zinaa.