Wakaazi wa kaunti ya Mombasa wanataka hatua za haraka kuchukuliwa kwa wizara zilizotajwa kuwa fisadi nchini.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakiongozwa na Saudina Kimani, mkaazi wa Jomvu, alisema kuwa wakuu wa wizara hizo sharti kuchukuliwa hatua za kisheria kwani wanafuja pesa za umma ovyo.

Siku ya Jumanne, aliongeza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kuwa pesa za wananchi zinafunjwa na watu wachache walioko mamlakani pasi kujali maslahi ya Mkenya mlala hoi.

Kauli hii inajiri baada ya Utafiti uliofanywa na tume ya maadili na kupambana na ufisadi humu nchini EACC kuonyesha kuwa wizara ya usalama wa ndani inaongoza kwa ufisadi humu nchini.

Wizara hiyo inaongoza kwa asilimia 40.3 ikifuatiwa na wizara ya afya kwa asilimia 14.3 huku wizara ya ardhi ikishikilia nafasi ya tatu kwa asilimia 11.

Wizara ya ugatuzi iko katika nafasi ya sita katika msururu huo ikiwa na asilimia 5.1.

Utafiti huo aidha unaonyesha kuwa asilimia 73.9 ya Wakenya wanaamini kuwepo kwa ufisadi humu nchini.

Kulingana na utafiti huo idara ya polisi ndio fisadi zaidi ikiongoza kwa asilimia 32.9.

Idara ya trafiki inachukua nafasi ya pili kwa asilimia 18.8 huku afisi za chifu nchini zikichukua nafasi ya tatu kwa asilimia 6.2.

Kaunti ya Muranga imeorodheshwa kuwa kaunti fisadi zaidi nchini ikiwa na alama ya wastani ya 3.78 ikifuatwa kwa karibu na kaunti ya Embu kwa alama ya wastani ya 2.53 Bomet 2.46 Kisii 2.41 na Wajir ikikamilisha kaunti tano zilizo fisadi zaidi nchini ikiwa na alama ya wastani ya 2.33.

Kulingana na utafiti huo kiwango kikubwa kilichowahi kutolewa huko Mandera ni elfu themanini huku elfu 52 kikiwa kiwango cha wastani kilichowahi kilichotolewa huko Garissa.

Huduma zilizotolewa hongo ni pamoja na afya asilimia 20.7 na ile ya usajili wa vitambulisho ikiwa na asilimia 18.4.

Ili kupata kandarasi, inambidi mtu atoe kiwango cha wastani cha zaidi ya laki mbili unusu huku wanaotafuta kazi wakishurutishwa kutoa hongo ya wastani ipatayo laki moja na elfu kumi na tano.

Utafiti huo wa EACC uliendeshwa kati ya Agosti 23 hadi Oktoba 23 mwaka jana katika kaunti 46 nchini isipokuwa kaunti ya Mandera ambapo watu zaidi ya elfu 5 walishirikishwa katika mahojiano ya ana kwa ana.