Wizara ya Afya katika kaunti ya Mombasa imehimizwa kuhakikisha kuwa inaangazia afya ya wakazi kwa kutibu visima vyote katika kaunti ya hiyo ili kuzuia mikurupuko ya maradhi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Afya katika Bunge la kaunti ya Mombasa Kibwana Swaleh Baya amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza kuenea kwa maradhi ya kiafya ikiwemo kipindupindu na homa ya maini.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumatano na mwanahabari huyo afisini mwake, Swaleh ambaye pia ni Mwakilishi wa Wadi ya Miritini amesema kuwa Kampuni ya kusambaza maji Mombasa lazima kuchukua jukumu hilo la kusambaza maji safi kwa wakazi, huku akiwahimiza wakazi kuchemsha maji na kudumisha mazingira safi ili kuepukana na magonjwa.
"Tunaitaka wizara ya afya kaunti ya Mombasa kuhakikisha kuwa inatibu maji wakazi wanayotumia hasa visima vya maji ili kuzuia kuenea kwa maradhi ya kipindupindu na haoma ya maini miongoni mwa wakazi," alisema Swaleh.
Kauli ya kiongozi huyo inajiri siku moja tu baada ya kuripotiwa zaidi ya watu 21 waliathirika na maradhi ya homa ya maini katika kaunti ya Mombasa, japo waendelea kupata matibabu katika hospitali kuu ya ukanda wa Pwani mjini Mombasa.
Picha: Mwenyekiti wa Kamati ya Afya katika Bunge la kaunti ya Mombasa Kibwana Swaleh Baya. Ameitaka Wizara ya afya kaunti ya Mombasa kutibu maji yote pamoja na visima vya maji kuzuia kushughudiwa kwa maradhi.