Wizara ya Afya imepewa changamoto kuhusiana na kujikokota kwake kupambana na funza ambao wamewaathiri maelfu ya watu kote nchini.
Akizungumza siku ya Jumatano katika eneo la Gesima kwenye kampeni dhidi ya funza, mwenyekiti wa shirika la Clean Health, Clinton Ouma, alihimiza serikali kufanya kazi na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ili kuangamiza funza.
Ouma alisema kwamba Wizara ya Afya haijatekeleza majukumu yake inavyostahili hali aliyosema imewanyima wanafunzi walioathiriwa na funza nafasi ya kuendeleza ndoto zao za masomo.
"Tumetembea katika maeneo mengi nchini na ninaweza thibitisha kwamba Wizara ya Afya haijafanya yakutosha kukabiliana na funza kwa kuwa wanafunzi wengi hulazimika kuacha shule kwa kuwa hawawezi tembea vizuri. Serikali inastahili kufanya kazi na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ili kukabiliana na funza hao," alisema Ouma.
Afisa huyo aidha alizishtumu serikali za kaunti kutokana na jinsi zinavyoendeleza kampeni zao za kuangamiza funza kwa kudai kuwa kampeni hizo huwafikia watu wa mijini na kuwatenga wale wanaoishi vijijini.
"Ni kweli kuwa serikali za kaunti zinafanya juhudi kuangamiza funza ila tu wanazingatia maeneo ya kibiashara huku wakiwatenga watu wengine vijijini,” alisema Ouma.