Wizara ya Afya nchini imeombwa kuchunguza wahudumu bandia ambao wamefungua zahanati za kuuza madawa kwenye maeneo ya mashambani ambao hawajahitimu kuwa wauguzi.
Muhudumu mmoja wa afya kwenye hospitali ya kibinafsi eneo la Ojola viungani mwa mji wa Maseno, Suzan Opondo ameitaka Wizara hiyo kuchunguza wote wanaouza dawa ambao wanawalaghai wananchi kwa kuwauzia dawa bandia ambayo wakati mwingine huatarisha maisha yao.
“Wizara ya Afya nchini inastahili kuweka mikakati kabambe ya kupigana na wahudumu bandia wa matibabu ambao wamesambaa mashinani hapa na wanawasababishia wananchi maafa na hasara,” alisema Opondo.
Opondo aongeza kuwa, “Wahudumu hao wanasababishia Wizara ya Afya nchini hasara kubwa kwa kuiba dawa ya Serikali ili kuendeleza biashara ya uuzaji wa dawa kwenye zahanati zao.”
“Hospitali nyingi nchini zinakosa huduma bora kwa wagonjwa kwa sababu dawa yanayotolewa na Serikali kutibu wananchi yanauziwa kwenye zahanati hizo,” aliongeza muhudumu huyo wa afya.
Opondo pia alifichua kwamba wahusika hao wengine wanaendeleza huduma za matibabu kama vile kudunga sindano, kuongeza maji na hata kulaza wagonjwa kisiri kwenye zahanati hizo.
Kumekuweko na visa mbali mbali vya vifo vinavyotokea na wagonjwa kutumia dawa ambayo hayaambatani na magonjwa yao, huku wakipewa dawa zaidi ya dozi bila kupimwa.
Baadhi ya wakazi katika eneo hilo pia walidai kuwa wengi wa wamiliki wa zahanati hizo hawakusoma na wamefoji barua bandia zinazoonyesha kuwa wamehitimu masomoni na kufuzu uuguzi.