Serikali imeanza harakati za kukagua na kufunga hospitali pamoja na maduka ya kuuza dawa yanayoendesha shughuli zake bila kufuata sheria.
Haya yanajiri baada ya kutokea lalama kuhusu baadhi ya wahudumu katika hospitali za humu nchini wanaovunja sheria wakati wa kutoa matibabu.
Akiongea mjini Mombasa wakati wa kikao na wadau wa afya, waziri wa afya nchini Cleopas Mailu alisema wizara yake itahakikisha watakaopatikana na hatia wanafunguliwa mashtaka.
“Tunajua hizi hospitali zipo na tutaanza kufanya ukaguzi ili kupata ushahidi. Lengo letu ni kuona kwamba hii idara inafanya kazi ipasavyo,” alisema Mailu.
Wakati huo huo, pia Mailu alitoa onyo dhidi ya vyuo vya kutoa mafunzo ya utibabu ambavyo havijasajiliwa.
Waziri huyo alisema hali hiyo imesababisha hasara kubwa kwani watu wengi wanaomaliza masomo yao katika vyuo hivyo wanaishia kuhangaika kwani stakabadhi zao hazitambuliki.
Aliongeza kuwa watu wengine wamechukua fursa hiyo kufanya biashara kwa kuanzisha vyuo hivyo kiholela.
“Tutahakikisha hivi vyuo havipo tena na vile vilivyopo vimesajiliwa, na kama hilo haliwezekani, itabidi tuvifunge,” alisema Mailu.
Waziri huyo alidokeza kuwa hatua hiyo italeta nafuu kwa wazazi wengi wanaowalipia watoto wao karo katika vyuo hivyo kisha baadae wanashindwa kupata ajira.