Wizara ya Ugatuzi na Mipango nchini imesema kuwa imemaliza mzozo uliokuwepo baina ya wizara hiyo na serikali za kaunti kuhusu mamlaka na uongozi.
Wizara hiyo ilisema kuwa tangu serikali za ugatuzi zilipoanza, kumekuwa na changamoto nyingi miongoni mwa viongozi wa kaunti kutokana na majukumu ambayo wengi walikuwa hawajazoea.
Akiongea katika Hoteli ya Serena mjini Mombasa siku ya Jumatatu, wakati wa kikao na kamati maalum ya seneti, Waziri wa Ugatuzi Mwangi Kiunjuri alisema kwamba wizara hiyo iliandaa kikao na magavana na kufanya makubaliano ya pamoja.
“Jambo lililokuwa na shida zaidi ni kuhusu mambo ya barabara lakini sasa tumekubaliana na magavana wanajua ni barabara gani iko chini ya kaunti na gani iko chini ya serikali kuu,”alisema Kiunjuri.
Kiunjuri alisema kuwa hakuna gavana yeyote anayefaa kwenda mahakamani kuhusu swala hilo kwani tayari tatizo hilo lilishatatuliwa.
Wakati huo huo, Kiunjuri alipinga madai kwamba wizara yake ina mzozo wa aina yoyote na bunge la seneti kama vile vyombo vya habari vimekuwa vikinukuu.
Waziri huyo aliongeza kwamba maseneta wametengewa fedha maalum ambazo zimejumuishwa katika bajeti ya mwaka ujao.
Aidha, alisema kwamba wizara hiyo imewasilisha rasmi sera mpya kwa kamati ya seneti zitakazowezesha utendakazi bora wa wizara hiyo.