Serikali imewahakikishia Wakenya kwamba imeweka mikakati dhabiti ya kuimarisha usalama kote nchini.
Msemaji wa Wizara ya Usalama nchini Mwenda Njoka alisema kuwa hatua ya serikali ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya usalama itasaidia katika kukabiliana na changamoto za kiusalama ambazo zimekuwa zikishuhudiwa.
Njoka alisema kuwa vyombo vya usalama nchini viko tayari kushirikiana na wanahabari kwa kuwapa ripoti ambazo wanazihitaji kwa wakati ufaao ili kuangazia taarifa zilizo na ukweli kuhusu masuala ya usalama.
“Serikali imejiandaa kikamilifu kuhakikisha kuwa usalama unaimarishwa kwani tuko tayari kushirikiana na vyombo vya habari wa kila eneo humu nchini kuwapa habari za Ukweli kuhusu usalama wa nchini,” alisema Njoka mjini Mombasa siku ya Ijumaa.
Njoka aliyasema hayo akiwa kwenye warsha ya mafunzo kwa wanahabari na maafisa wa usalama mjini mjini Mombasa kuhusu wajibu wa vyombo vya habari katika kukabiliana na ugaidi na misimamo mikali.
Warsha hiyo imeandaliwa na Baraza la Vyombo vya Habari nchini na shirika la IMS.