Wizara ya Utalii nchini kwa ushirikiano na wadau wa sekta hiyo wameahidi kuimarisha sekta ya utalii katika bandari ya Mombasa kwa kujenga jumba la kupokea watalii wanapowasili katika bandari hiyo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Waziri wa Utalii nchini  Najib  Balala amesema kuwa tayari shilingi milioni 100 kutoka kwa Halmashauri ya Bandari nchini KPA na shilingi milioni 100 kutoka kwa wizara hiyo zimetengwa kugharamia ujenzi wa jumba hilo pamoja na uboreshaji wa eneo la Dongo Kundu.

"Tayari fedha zimetengwa kushughulikia ujenzi huo na tunapanga shughuli hiyo kuanza rasmi kabla ya mwezi wa tisa ili kuhakikisha kuwa sekta ya utalii nchini inaimarika," alisema Balala siku ya Jumanne katika bandari ya Mombasa. 

Amesema kuwa jumba hilo litatumika kuwasajili watalii wanaowasili nchini na wale wa kinyumbani katika eneo la kuegesha meli la kwanza katika bandari hiyo, huku akisema kuwa iwapo sekta ya uchukuzi itaimarisha ujenzi wa miundo msingi, basi sekta hiyo haitakuwa na changamoto.

Akigusia swala la usalama, Balala ameishinikiza idara ya usalama nchini kuhakikisha kuwa inakabiliana kikamilifu na maharamia ili kuhakikisha kuwa bahari hindi ya Pwani ya Kenya na Somalia inakuwa na usalama dhabiti.

Kwa upande wake Kaimu mkurungenzi mkuu wa Halmashauri ya Bandari nchini KPA Catherine Wairi ameahidi kushirikiana na wadau wote wa sekta ya utalii kuhakikisha kuwa sekta ya utalii nchini inarejea kama ilivyokuwa hapo awali.