Wafugaji wa mifugo kutoka kaunti za Kisii na Nyamira watakuwa na sababu ya kutabasamu, baada ya shirika moja la kutengeza vyombo vya usalama kuahidi kuwaletea vidude vya kufuatilizia na kuchunga ng’ombe na mbuzi wao iwapo wataibwa.
Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo; Agmond International Charles Anunda, akiongea na mwandishi wetu alisema kuwa wanalenga wakulima kwa sababu ya wizi wa mifugo haswa ng’ombe na mbuzi, ambao umekuwa ukishuhudiwa kwenye mpaka wa Kisii na Transmara, amabo umesababisha vita baina ya jamii za Wakisii na Wamaasai kwa mda mrefu.
Anunda alisema kuwa shirika lake litakuwa na kongamano kwenye chuo cha Multmedia jijini Nairobi tarehe 8 na 9, na baadaye maeneo ya Gusii kukutana na wakulima kuwapa ujumbe huo na jinsi ya kupata bidhaa hizo.
Miongoni mwa bidhaa hizo ni vidude ambavyo vitakuwa vikiwekwa kwenye mwili wa ng’ombe na mbuzi ili kufuatilia mifugo hao iwapo wameibwa, na kamera za usalama maarufu kama CCTV ambazo zitawekwa katika zizi za wanyama ili kurekodi na kuangaza matukio pamoja na visa vya wizi na wezi hususan nyakati za usiku.
Mkurugenzi huyo aidha alidokeza kuwa kampuni hiyo ya Agmondi International itauza ala hizo kwa bei nafuu, na wafugaji wote wawe tayari kufaidi kutokana na bidhaa hizo ili kuleta suluhu kwenye suala la wizi wa mifugo ambalo umekuwa sugu kwenye maeneo hayo.