Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Changamoto ya ukosefu wa usalama inaonekana kutikisa hatua zilizopigwa za kuimarisha umoja humu nchini huku chanzo kikisemekana kutokana na ukosefu wa maadili mema katika jamii.

Kulingana na mkurugenzi mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la HURIA Yusuf Lule alisema kuwa kuongezeka kwa vikundi vya uhalifu vinavyohangaisha wakaazi katika kaunti ya Mombasa ni ishara ya kuwa kuna haja ya kujumuika kwa kila mmoja ili kufanikisha utulivu mjini Mombasa.

Lule aliongeza kuwa ni sharti jamii kulivalia njuga swala la mafunzo ya maadili mema hususan kwa vijana iwapo wanataka kukabiliana na utovu wa usalama katika kaunti hii ya Mombasa.

“Wazazi lazima wajumuike katika kutoa mafunzo na malezi bora ya kimaadili kwa vijana na wana wao iwapo wanatazamia kuimarisha swala la usalama katika kaunti ya Mombasa,” alisema Lule.

Aidha, amesisitiza kuwa wazazi,vyombo vya usalama na viongozi serikalini wanapaswa kufanya mazungumzo ya kina ili kutafuta suluhu ya kudumu kwa donda hilo la uhalifu.

Ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana umetajwa kama chanzo cha wao kujihusisha na vitendo vya kihalifu na kujiunga na vikundi vilivyopigwa marufuku.

Vikundi hivyo vinasemekana kutekeleza madhila hayo bila uwoga hata nyakati za mchana licha ya onyo kutolewa na vyombo vya usalama.

Hata hivyo kwa upande wake Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba aliwataka maafisa wa usalama kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaotishia kuvuruga usalama na utulivu Mombasa.

Ahadi iliyotolewa na kamanda wa polisi katika kaunti ya Mombasa Francis Wanjohi ya kusambaratisha kikundi cha “wakali kwanza” ifikiapo mwezi Februari mwaka ujao bado inasubiriwa kama itatimia.