Zaidi ya wakulima 20 wa Ng’ombe wa maziwa kutoka eneo la Mwakirunge kaunti ya Mombasa wanakadiria hasara kubwa baada ya bidhaa yao ya maziwa kukosa kununuliwa kwa muda wa siku nne na kuharibika.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakulima hao ambao huuza maziwa kwa kampuni mbalimbali za maziwa hapa Mombasa sasa wanasema kuwa iliwalazimu kuuza zaidi ya lita elfu mbili za maziwa kwa wateja wa rejareja kuhakikisha kuwa bidhaa hiyo haiharibiki.

Hatua hiyo hata hivyo haikuwasaidia kwani mengi ya maziwa hayo yaliishia kuharibika kwenye mitungi ya kuhifadhia.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa chama cha wakulima wa maziwa eneo hilo Japhet Mbae, wakulima hao walisema kuwa kuharibika kwa bidhaa hiyo kumechangiwa na baadhi ya kampuni zinazonunua maziwa kupunguza bei ya kununua bidhaa hiyo, hatua ambayo ilipelekea wao kususia kuwauzia.

Akitoa mfano wa kampuni ya Brookside, Mbae alidokeza kwamba imepunguza bei ya lita moja ya maziwa kutoka shilingi arubaini hadi shilingi ishirini kwa lita, hatua ambayo ameitaja kama ya kuwakandamiza kiuchumi.

Hata hivyo wametoa wito kwa serikali ya kaunti kuwasaidia kwa kuwatafutia soko mbadala ili waweze kuuza bidhaa hiyo.