Naibu chifu wa kata ndogo ya Nyamakoroto lokesheni ya Karantini, wadi ya Gesima Robert Monda, aliwaongoza wanakijiji kumwaga zaidi ya lita 3,000 za pombe haramu.
Akiongea siku ya Alhamisi katika msako huo katika sehemu ya Nyamakoroto, Monda alisema kuwa atahakikisha kuwa pombe haramu imeisha katika kata hiyo kutokana na agizo la raisi na chifu wake.
Aidha, aliwaonya wagema wote haswa wanaotoa hongo kwa maafisa wa polisi ili kuendelea na biashara hiyo huku akisema yeyote atakaye patikana akitoa hongo atachukuliwa hatua ya kisheria kwani hatawaruhusu wagema kuendelea kutengeneza pombe hiyo haramu.
“Mgema atakaye toa hongo kwa polisi atakuwa akitupa pesa zake kwa kuwa wakati wa kutoa hongo umeisha. Hatuwezi toa hongo ili kuangamiza vijana wetu na pombe haramu. Atakaye patikana atachukuliwa hatua ya kisheria," alisema Monda.
Naibu Chifu Monda ambaye aliandamana na wazee wa vijiji na wanakijiji walishirikiana kwa msako huo na kusema kuwa wataendelea kushirikiana ili kuhakikisha kuwa pombe hiyo imeisha katika lokesheni yao.
Duke Osase, mkazi, alisema kuwa watashirikiana na naibu chifu na machifu wote ili kukomesha pombe hiyo na kuwaomba wakazi wengine kujitolea ili kuunga mkono msako huo.
Osase alisema kuwa pombe hiyo ikiisha katika lokesheni hiyo maendeleo yatanawiri kwa kuwa watu watakuwa wanajihusisha na kazi ya maana badala ya kubugia pombe kila siku.
kwa sasa wamewaomba wabunge wa Kaunti ya Nyamira kuungana na machfu katika msako huu ili kuhakikisha kuwa pombe haramu imeisha katika kaunti hiyo.