Takriban walimu mia sita kutoka Mombasa wametuma maombi ya ajira katika viwango vya ualimu wa shule za msingi.
Akithibitisha ripoti hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa TSC tawi la Mombasa Bi Mwanasiti Mwakibonje, amesema walimu ambao watafaulu kwenye mahojiano watalazimika kujaza fomu ambazo zitadhihirisha kuwa wamepitia mahojiano.
Mwakibonje alisema kuwa fomu hizo zitatumwa kwenye makao makuu ya TSC jijini Nairobi.
Kwa upande wao, walimu waliojitokeza kwenye mahojiano hayo waliitaka tume hiyo kuzingatia viwango vya elimu haswa alama waliyopata vyuoni pamoja na uzoefu wa kazi.
Walihu hao walisema kuwa hatua hiyo itasaidia pakubwa ukuaji wa elimu katika Kaunti ya Mombasa.
Aurelia Ngina, mmoja wa walimu aliyefika kwenye mahojiano hayo, alisema kuwa amekuwa akisaka kazi hiyo kwa miaka zaidi ya minne.
Aliitaka Tume ya TSC kuzingatia walimu waliohitimu masomo miaka ya hapo awali.
“Itakuwa kigezo muhimu kwa TSC kufuatilia jambo hilo ili kupata walimu ambao wanatajriba ya kutosha,” alisema Ngina.
Kwa upande wake, Mourice Kahindi alipinga vikali hoja hiyo akisema itawafungia nje baadhi ya walimu ambao walihitimu hivi karibuni.
“Kuna walimu ambao wanajua kufundisha vizuri ikilinganishwa na wale waliomaliza masomo ya ualimu miaka kadhaa iliyopita,” alisema Kahindi.
Bi Mwanasiti hatahivyo aliwahakikishia walimu hao kuwa kanuni zote na sheria zilizowekwa kwenye zoezi hilo zitafuatiliwa ili kuhakikisha kuwa serikali inapata walimu waliobora zaidi.