Zaidi ya wasichana 1,000 ambao awali walikuwa makahaba mjini Eldoret wamesaidiwa kurekebisha tabia.
Wasichana husika wamekuwa wakipokea mafunzo ya kurekebisha maisha yao kupitia kwa shirika la SOLASA katika mtaa wa Langas mjini Eldoret.
Mkurugenzi wa shirika hilo Elizabeth Shako alisema shirika hilo limekuwa likiwatafuta wasichana hao ambao awali walikuwa makahaba na kuwapa ushauri nasaha kuhusu jinsi ya kurekebisha tabia na namna ya kukabiliana na changamoto ya maisha.
Akihutubu wakati wa sherehe ya kufuzu kwa baadhi ya wasichana hao mtaani Langas Shako alisema wengi wa wasichana hao huingilia biashara hiyo kutokana na ugumu wa maisha na malezi duni.
Ili kuzuia wasichana zaidi kujitosa katika uraibu wa dawa za kulevya na ukahaba Shako aliwataka wazazi kuwajibika vilivyo na kuachana na biashara ya chang'aa na dawa za kulevya ili kuwalea watoto wao katika mazingira bora.
Mkurugenzi huyo alisema kwa sasa, wasichana hao wamerekebisha tabia na kuanza kujihusisha na biashara halali ya kujikimu maishani ambapo wengine wao wameamua kurudi shuleni ili kuendlea na masomo yao.
"Wasichana hawa wana vipawa vingi ambavyo vimekuwa vikiozea mitaani; wengi wao kwa sasa wamepokea mafunzo ya kiufundi, biashara, ususi wa nywele, uzalishaji wa vinywaji kutoka kwa matunda miongoni mwa mafunzo mengine," alisema.
Aliwaomba wahisani mbalimbali kusaidia kituo chake kuweza kuendelea kusaidia wasichana husika ili wajikimu maishani.
Mbali na kuwasaidia wasichana hao kituo hicho pia kimewasaidia akina mama zaidi ya 2,000 ambao walikuwa wagemaji na wauzaji pombe haramu kurekebisha tabia na kuanzisha biashara mbadala.