Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika lenye makao yake Mombasa limedai kuwa zaidi ya watu 20 wamepotea katika hali ya kutatanisha.
Haki Afrika imesema kuwa idadi hiyo imerekodiwa ndani ya mwaka mmoja uliopita, huku ikijumuisha wanawake na wanaume waliohusishwa na visa vya ugaidi.
Afisa wa shirika hilo Bw Francis Gamba, amesema kuwa visa kama hivyo vimeongezeka hasa katika ukanda wa Pwani.
Gamba alisema kuwa serikali lazima ijitahidi kukabiliana na swala hilo.
Aidha, afisa huyo alisema amethibitisha kuwa miili ya watu imekuwa ikipatikana katika Mbuga ya wanyama ya Tsavo baada ya kuripotiwa kupotea.
“Watu wanaojitambulisha kama maafisa wa polisi huwatia mbaroni wananchi kisha kuwapoteza katika hali ya kutatanisha. Tulipata miili ya Samir Khan na Meshack Yebei katika Mbuga ya Tsavo,” alisema Gamba.
Aidha, inadaiwa kuwa baadhi ya jamii katika ukanda wa Pwani zimekuwa zikihofia kupiga ripoti kwa vitengo husika serikalini baada ya wapendwa wao kupotea katika hali isiyofahamika, zikihofia kuhangaishwa badala ya kupewa usaidizi muafaka.
Shirika la Haki Afrika limekuwa katika mstari wa mbele kutetea haki za kibinadamu na huduma zake ziliwahi kutatizwa hapo awali, baada ya akaunti za shirika hilo kufungwa kutokana na tuhuma za kufadhili makundi ya kigaidi.