Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kamati maalum inayosimamia shughuli za maandalizi ya ziara ya baba mtakatifu katika Kanisa Katoliki la Jimbo kuu la Mombasa limepanga kusajili zaidi ya watu elfu mbili watakaosafari jijini Nairobi kuhudhuria misa takatifu itakayoongozwa na Papa Francis.

Kulingana na Kiongozi wa kamati hiyo, Padri Wilbard Lagho, kati ya waumini hao elfu mbili, 700 kati yao ni vijana watakaokuwa katika msafara huo wakieneza ujumbe wa amani kwa taifa la Kenya kama njia mojawapo ya kuwaunganisha wakazi wa Pwani.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, Padri Lagho, ambaye pia ni Naibu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Mombasa alisema kwamba hakuna atakayeruhusiwa kujumuika katika msafara huo iwapo hajasajiliwa na kamati hiyo ili kuepukana na visa vya uhalifu.

Padri Lagho amesema kwamba wanatarajia mabasi ya waumini hao 68 kutoka jimbo la Mombasa, ikiwemo kaunti za Mombasa, Kwale, Taita Taveta na Kilifi, huku akiongeza kwamba kamati hiyo itazingatia zaidi vyeti vya kitaifa, vile vya Kanisa hilo na vyeti vingine muhimu kabla ya wakristo hao kuruhusiwa kusafari.

Padri Lagho aidha amewataka wahisani kujitokeza na kuwasadia na mabasi ya uchukuzi wa umma, vyakula, maji na bidhaa zingine za kuwasaidia wakati wa msafara.

"Tunatarajia zaidi ya mabasi 68 yatakayobeba waumini zaidi ya 2,000 wa kanisa katoliki jimbo la Mombasa kutoka katika parokia 25 za jimbo hili kuelekea kule jijini Nairobi kuhudhuria ibada maalum ya Papa Francis, na tunaomba wahisani pia kujitokeza na kutusaidia na magari na chakula wakati wa msafara huo kwani utakuwa tunaeneza ujumbe wa amani," alisema Lagho.