Zoezi la kusajili makurutu watakaojiunga na Idara ya Polisi nchini limeanza katika kaunti zote nchini.
Vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini walijitokeza katika vituo vilivyo karibu nao siku ya Jumatatu ili kujaribu bahati yao katika shughuli hiyo inayong’ang’aniwa na wengi wenye hamu ya kujiunga na idara ya usalama.
Katika kaunti ya Mombasa, zoezi hilo lilifanyika katika Uwanja wa Mvita ambapo vijana kumi kutoka eneo hilo watateuliwa kujiunga na kikosi cha polisi wa utawala, huku 20 wakiteuliwa katika kikosi cha polisi wa kawaida.
Akiongea baada ya zoezi hilo kukamilika, Kamishna wa huduma kwa polisi Murshid Mohamed alisema kuwa wananchi wanafaa kuwa na subira kabla kujua ni akina nani waliochaguliwa katika uteuzi huo.
“Majibu hayawezi kutoka leo kwa sababu hata katika kituo hiki hatujui ni idadi gani tutachukua. Zoezi lote likishakamilika ndipo tutawaeleza vizuri,” alisema Mohamed.
Mohamed aliongeza kuwa itachukua muda wa wiki mbili kabla kubaini wale waliofaulu katika shughuli hiyo.
Hata hivyo, inadaiwa idadi ndogo ya vijana walijitokeza katika zoezi hilo mwaka huu katika Kaunti ya Mombasa, ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Kamishna mkuu wa tume ya huduma kwa polisi nchini Johnstone Kavuludi akitangaza uzinduzi wa zoezi hilo hapo awali, alisema kuwa tume yake imejitayarisha vya kutosha kuhakikisha hakuna visa vya udanganyifu.