Usajili wa Makurutu katika Idara ya Magereza ambao ulitekelezwa siku ya Jumatano asubuhi katika Uga wa michezo wa Gusii ulikamilika bila utata wowote wala ufisadi.
Akiongea na Waandishi wa Habari baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Afisa aliyesimamia shughuli hiyo Sajenti Mkuu Cyrus M'mtumutambo aliwashukuru Makurutu wote walioshiriki katita usajili huo na kuwataka wawe waadilifu kwani kazi ya Polisi ni kuhudumia jamii kwa ujumla.
"Nawaomba muwe watiifu na kudumisha maadili ya kazi, msiwe watu wa kushawishiwa kuchukua hongo wala kutoa hongo. Huu ni wito hivyo basi inakuhitaji muwajibikia jamii na wale wafungwa mnaoenda kuhudumia baada ya mafunzo,” alishauri M'mtumutambo.
Naye Naibu Afisaa Mkuu wa Idara ya Magereza Kisii Esther Omundi ambaye alihudhuria shughuli hiyo ya kusajiliwa kwa Makurutu aliwapongeza wazazi pamoja na Makurutu kwa kujiepusha na ufisadi ilivyokuwa hapo awali, kitendo ambacho alisema imenyima vijana wanaofaa kazi hiyo na kuwapa wahalifu nafasi akiongeza kuwa Serikali imejitolea kupigana na ufisadi.
Mmoja wa wazazi ambaye mtoto wake alifuzu Joash Moranga aliwashukuru Maafisa wote waliofanikisha shughuli hiyo na kuonyesha furaha yake baada ya kijana wake ambaye alikosa nafasi ya Makurutu wa Polisi mwezi Aprili kufaulu wakati huu.
Makurutu wanne waliweza kufaulu katika kituo hicho cha Uga wa michezo wa Gusii ambazo ni nafasi zilizo tengewa eneo Bunge la Kitutu Chache.