Serikali ya kaunti ya Nyamira kupitia afisa mkuu wa afya katika kaunti hiyo Douglas Bosire amesema lengo lao ni kutoa chanjo ya Polio kwa idadi ya watoto 130,961 walio chini ya miaka mitano katika kaunti hiyo.
Akizungumza siku ya Alhamisi mjini Nyamira, Bosire alikiri kuwa lengo la serikali katika kaunti ya Nyamira ni kuchanja idadi kubwa ya watoto kuhakikisha hakuna waathiriwa katika siku za usoni kwa ukosefu wa chanjo hiyo ya Polio.
“Hapa Nyamira lengo letu kwa kutoa chanjo kwa watoto walio chini ya miaka mitano ni 130,961 kwa siku tano zijazo kuanzia siku ya Jumamosi wiki hii,” alisema Bosire.
Bosire aliwahimiza wakazi wakiwemo wazazi na wahisani kushirikiana pamoja na maafisa wa sekta ya afya ili kukinga magonjwa mbalimbali ambayo husabishwa na ukosefu wa chanjo hiyo
“Ugonjwa wa Polio ni ugonjwa wa kawaida kwa watoto ambao unaweza kusababisha kupooza na kuleta madhara hatari, lakini tunahitaji kuzuia hayo tuwaleta watoto kwa wingi wapate chanjo hiyo,” aliongeza Bosire.