Takriban vijana 31 kutoka kaunti ndogo ya Subukia walibahatika kusajiliwa kama makurutu katika kikosi cha polisi huku kukiwa na madai kuwa zoezi hilo halikufanyika kwa njia ya haki.

Share news tips with us here at Hivisasa

 Mary Kigen, mzazi, ambaye mwanawe alitarajia kusajiliwa katika zoezi hilo alilalamika kuwa alichujwa kwa sababu alikuwa amejiunga na kukamilisha kozi yake katika huduma kwa vijana wa taifa National Youth Service (NYS).

“Mwanangu licha ya kufanyiwa ukaguzi na kupita, aliambiwa kuwa kwa sababu amekamilisha masomo yake katika NYS, anayo nafasi ya kupata kazi hivyo basi awape nafasi wengine. Mimi najiuliza kwani huwezi pata kazi kwa kuwa umekamilisha mafunzo katika NYS?” aliuliza Kigen.

Naye Kevin Kamau ambaye alifika katika uwanja huo wa michezo kujaribu bahati yake alielezea hisia zake.

“Kwa kweli usajili huo huakufanywa kwa njia ya uwazi. Niliondolewa katika hatua za mwisho na sikuelezwa sababu ya kuondolewa kwangu,” alisema Kamau.

Hata hivyo, kamanda wa kikosi cha polisi aliye tumwa kusimamia zoezi katika eneo hilo Lazarus Opicho, kutoka makao makuu jijini Nairobi, alisema zoezi hilo halikuwa na dosari zozote na lilifanyika kwa njia ya uwazi.

“Tulizingatia umri na elimu. Na nina wapongeza wakazi wa Subukia kwa ushirikiano wao mzuri katika kufanikisha zoezi hili,” alisema bwana Opicho.

Jumla ya vijana 1,500 walijitokeza kujaribu bahati yao. 

Opicho aliwahimiza walio sajiliwa  kuwa na nidhamu ya juu kwani watafanyiwa ukaguzi zaidi kabla ya kujiunga na vyuo husika.

Makurutu hao wanatarajiwa kuripoti katika vyuo hivyo siku ya Ijumaa wiki hii.